MWANJALI AMUWAHI IBRAHIMU AJIBU

MASHABIKI wa Yanga wanachonga sana mitaani kwa sasa kutokana na majembe ya maana yaliyotua kikosini mwao akiwamo Ibrahim Ajibu aliyeungana na akina Donald Ngoma, Obrey Chirwa na Amissi Tambwe kuipa makali safu yao ya mbele.

Lakini kama Yanga inatarajia mteremko katika pambano la Ngao ya Jamii dhidi ya Simba litakalopigwa Agosti 23 Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam, pole yao. Habari ni kwamba yule beki kisiki Mzimbabwe Method Mwanjali karudi mapema.

Mwanjali aliyekuwa majeruhi kwa muda mrefu Simba, amepona na ameanza mazoezi sambamba na nyota wenzake waliopo kambini Afrika Kusini.

Kama hujui, Mwanjali ndiye aliyechangia kwa kiasi kikubwa kuinyima Yanga mabao katika pambano la duru la kwanza la Ligi Kuu Bara msimu uliopita lililochezwa Oktoba Mosi, 2016 na kumalizika kwa sare ya bao 1-1.

Katika pambano hilo, Yanga ilipata bao lake la utatanishi lililofungwa kwa kutengenezwa na mkono na straika wake, Amissi Tambwe kabla ya Shiza Kichuya kuisawazishia Simba bao la kideoni kwa mpira wa kona ulioenda kimiani moja kwa moja zikiwa zimesalia dakika tatu kabla ya mchezo huo kumalizika.

Mwanjali hakuwepo kwenye pambano la marudiano lililopigwa Februari 25 ambapo Yanga ilikufa kwa mabao 2-1. Beki huyo aliumia mechi mbili kabla ya watani hao kurudiana, hivyo kurudi kwake kikosini Yanga haitafurahia.

Beki huyo anayecheza kwa akili na maarifa sambamba na kukaba nafasi ya straika aliyepo mbele yake, huenda akawatibulia Yanga kaika mechi ya Ngao ya Jamii kwa sababu anamjua vizuri Ajibu aliyekuwa naye kikosini Msimbazi.

Kocha Msaidizi wa Simba, Jackson Mayanja, alisema beki mkongwe huyo anaendelea vema kupiga tizi na wenzake kambini baada ya kupona kabisa tatizo lake la goti ambalo aliumia msimu uliopita katika mechi za mzunguko wa kwanza wa Ligi Kuu Bara walipovaana na Prisons.

“Mwanjali anaendelea vizuri na anafanya mazoezi kama wachezaji wengine na kwa maelezo ya daktari tunaweza kumtumia kwani ameshapona kabisa,” alisema Mayanja raia wa Uganda.

Omog hana presha

Katika hatua nyingine Kocha Mkuu wa Simba, Joseph Omog, amesema hawana presha yoyote na kile kinachofanywa na watani zao na badala yake wanaendelea na mambo yao ikiwamo kuwafua vijana wake waive tayari ya vita ya Ligi Kuu Bara.

Simba inaendelea kupiga tizi la kufa mtu katika mji wa Johannesburg, ikijiandaa kwa ligi na michuano mingine iliyopo mbele yao likiwamo Kombe la Shirikisho Afrika.

Kocha Omog aliliambia Mwanaspoti kuwa kwa usajili uliofanywa na Yanga wala hauwatii presha kwa vile anaamini maandalizi wanayoyafanya Sauzi ni mazuri na muhimu kuliko watani zao.

Omog alisema Yanga wamefanya usajili wa kawaida na hata watakapokutana nao anaamini Simba itakuwa bora zaidi.

“Huku tulipo sisi kuna hali ya hewa ya baridi ambayo huwajenga wachezaji mara mbili ya ubora ambao wangeupata kama wangefanya mazoezi eneo la joto, hivyo kwa maandalizi yetu, Yanga haitutii presha kabisa,” alisema.

“Kambi inaendelea vizuri na kubwa la kuvutia ni wachezaji wapya na waliotangulia mapema wanapokea kwa kiasi kikubwa kile ninachowapatia.”

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MBARAKA YUSUPH BADO HALI TETE

NIYONZIMA AAHIDI ZAWADI KWA KAZIMOTO