JAZWA UJAZWE

YANGA wamesikia nyodo za Simba waliokuwa wamepiga kambi Afrika Kusini, wakacheeka halafu wakawajibu kwamba kwa tizi lililopigwa hapo Morogoro lazima Mnyama ajazwe.
Yanga wanatamba kwamba wana vikosi viwili matata ambavyo kimoja kinaweza kupiga mechi ya Simba pale Uwanja wa Taifa na kingine kikasafiri kwenda mkoani kucheza mechi nyingine ya ligi hiyo hiyo na mambo yakaenda.
Kocha wa Riadha wa Brunei, ambaye pia mnazi wa kulia wa Yanga, Suleiman Nyambui, amedai kwamba amekiangalia kikosi cha Simba na mastaa wote anawajua wala hakimpi presha na haoni jinsi watakavyochukua ubingwa mbele ya Yanga hii.
Lakini nahodha wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’kapigilia msumari kwamba kwa tizi walilopiga hapo Morogoro hana wasiwasi hata kidogo na kikosi chake na anaamini kwamba mambo yatakuwa freshi na mashabiki watakenua meno yote.
Vigogo wa usajili wa Yanga, wamemrahisishia kazi kocha George Lwandamina kwa kumpatia orodha ya mastaa ambao anaweza kuwatumia kusuka vikosi viwili vya maana na anaweza kuvipa kazi mbili tofauti na zikatekelezeka bila kuleta athari kwa timu ambayo msimu ujao itashiriki Ligi ya Mabingwa Afrika, Ligi Kuu Bara, Kombe la FA na Kombe la Mapinduzi.
Hiyo ina maana kwamba Yanga inaweza kuwa na kikosi cha maana kilichosheheni wakongwe, wazoefu na wachezaji walioko kwenye fomu ambao wanaweza kucheza dhidi ya Simba au Al Ahly ndani ya Uwanja wa Taifa na kikapatikana kikosi kingine ambacho kinaweza kucheza na Lipuli au Ndanda kwenye mechi ya ligi kule Mtwara au Iringa.
Mziki wa kwanza wa Yanga unaweza kuanza na kipa ngongoti, Youthe Rostand, Juma Abdul, Gadiel Michael, Mnigeria Tony Okoh, Kelvin Yondani, Mcongo Kabamba Tshishimbi, Mzambia Obrey Chirwa, Thaban Kamusoko, Donald Ngoma, Rafael Daud na Ibrahim Ajibu.
Mashine zingine zinazoweza kuunda kikosi kingine cha pili cha maana ambacho kinaweza kuwanyoonya watu kwenye Ligi ni kipa mahiri Beno Kakolanya, beki mtata Hassan Kessy, Haji Mwinyi, Abdallah Shaibu ‘Ninja’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Said Juma ‘Makapu’, Juma Mahadh, Pius Buswita, Amissi Tambwe, Mateo Anthony na Geofrey Mwashiuya.
Lakini huku nje kutakuwa na vifaa vingine vitakavyokuwa vinapasha kwa fujo tayari kuchukua namba ambavyo ni Ramadhan Kabwili, Said Musa, Ibrahim Yahaya, Emannuel Martin na Yusuph Mhilu.
Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Yanga, Hussein Nyika, alisema: “Yanga sasa inaangalia zaidi mashindano ya kimataifa ambayo ili ufanye vizuri ni lazima uwe na kikosi kilichokamilika kila idara kama kocha alivyopendekeza kwenye ripoti yake. Hatufanyi usajili kwa kukurupuka bali tumeimarisha maeneo ambayo yalionyesha udhaifu msimu uliopita.”
MSIKIE CANNAVARO
Cannavaro ambaye ni nahodha wa Yanga ametamka kwamba kwa mazoezi waliyopigishwa katika kambi yao ya Morogoro yalikuwa ni zaidi ya magumu lakini sasa wako tayari kukutana na yeyote na kupiga mpira mwingi.
Alisema miili yao sasa imekuwa tayari kucheza mpira na kwamba kikosi chao sasa kimeimarika kwa kila mchezaji kuwa tayari kuvaa jezi ya timu hiyo na kufanya kweli ambapo kwa kuanzia watafanya kweli dhidi ya Singida United leo.
“Tumekuwa na kambi ya mafanikio tumefanya mazoezi magumu sana, lakini haya ndiyo mazoezi yanayotakiwa kipindi hiki tupo tayari kukutana na yeyote kila mchezaji sasa anahamu kubwa ya kucheza soka,”alisema Cannavaro.
“Tunajua tunarudi jijini Dar es Salaam na tutacheza mechi mbalimbali lakini kwa hali ninayoiona kuna timu inaweza kupigwa nyingi hilo wajiandae nalo wasije kusema wamehujumiwa hilo linatokana na jinsi tulivyotayari.”
NYAMBUI NAYE KANENA
Katibu wa zamani wa Riadha Tanzania (RT), Seleiman Nyambui, anayefundisha mchezo huo huko Brunei akiwa kocha wa kulipwa, amesema kwa namna alivyoufuatilia usajili wa Yanga, unaonyesha bado wataendelea kutwaa mataji ya Ligi Kuu.
“Kati ya mambo waliyoyafanya Yanga kwenye usajili ni kuepuka kusajili wachezaji wa mashabiki,wameangalia mahitaji muhimu, lakini Simba nimeangalia safu ya kiungo wapo wachezaji zaidi ya sita, hii inamanisha kama wanahofu na watani wao,” alisema.
Nyambui alisema hazungumzii kishabiki bali anaangalia mustakabali wa maendeleo ya soka hasa kwa klabu kongwe Simba na Yanga, kujitahidi kufanyika kioo dhidi ya timu zinazoshiriki ligi kuu.
“Ni kweli nimeanza kuishabikia Yanga mwaka 1974, enzi za kina Sunday Manara, lakini ninaposimama kama mwanamichezo siwezi kusimamia timu moja, lengo ni kuona Tanzania inasonga mbele katika sekta zote,” alisema.
Lakini alimtaja Edibily Lunyamila kwamba ni alama ya wachezaji wazawa wanaodhihirisha kwamba nchi ina vipaji, isipokuwa viongozi ni wavivu kuviendeleza.
“Huwezi kusema unaweza kuwa na timu nzuri kwa kunyakua wachezaji kutoka kwa wapinzani na ndiyo maana wengi wanaotoka mikoani wana ndoto za kucheza Simba na Yanga na si nje ya nchi, hii inaonyesha soka lilivyodumaa,” alisema.

Maoni

Machapisho maarufu kutoka blogu hii

MBARAKA YUSUPH BADO HALI TETE

NIYONZIMA AAHIDI ZAWADI KWA KAZIMOTO